Kufuatia kutokea kwa ajali mbaya iliyosababisha vifo vya wanafunzi 33 na waalimu wawili na dereva wa gari hilo, Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), limetoa rambirambi ya Sh. 500,000 kwa walengwa waliopoteza watoto katika ajali hiyo.

Ajali hiyo ilitokea Ijumaa maeneo ya Rhotia marera wilayani Karatu mkoani Arusha ambapo ilisababisha vifo vya wanafunzi 33, walimu wawili na dereva wa shule ya Lucky Vincet iliyopo Jijini humo.

Aidha, Wanafunzi na waalimu hao walikuwa wakielekea shule ya Tumaini kwa ajili ya kufanya mtihani wa ujirani mwema.

Salamu za rambirambi za TFF  zimetolewa na rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Jamal Malinzi ambapo ameungana na viongozi mbalimbali kuomboleza msiba huo.

“Mtazamo wetu kwa sasa ni kuendeleza soka la vijana, tena hasa wale walioko mashuleni hivyo vijana wale ni sehemu ya kutimiza ndoto za TFF katika mpira wa miguu hapo baadaye, tunakubali haya yote kwa kuwa ni ya Mwenyezi Mungu ndiye anayejua siri,” amesema Malinzi.

Hata hivyo, Malinzi amewataka wanafamilia wote wa mpira wa miguu kuwaombea marehemu wote wapumzishwe mahali pema peponi.

 

Lord Eyez afunguka tena kuhusu dawa za kulevya
?Live: Maombolezo kitaifa ya wanafunzi zaidi ya 30 waliofariki katika ajali Arusha