Naibu Katibu Mkuu wa CUF – Bara, Magdalena Sakaya ameonya mpango wa Katibu Mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad kushiriki kufunga Kampeni za kumnadi mgombea ubunge wa jimbo la Liwale, Mohammed Mtesa.
Hatua hiyo imetokana na taharuki iliyoibuka kati ya pande mbili za chama hicho zilizo na mgogoro, yaani upande wa Mwenyekiti wa chama hicho anayetambuliwa na ofisi ya Msajili wa vyama vya siasa, Profesa Ibrahim Lipumba na upande wa Maalim Seif.
Profesa Lipumba alikuwa wa kwanza kufungua kampeni za kumnadi Mtesa kama mgombea wa chama hicho, lakini upande wa Maalim Seif kupitia kwa mbunge wa Kilwa, Suleiman ‘Bwege’ Bungala wametangaza kushiriki pia kampeni hizo.
“Mgogoro upo lakini tunaunganishwa na mgombea wetu kwenye uchaguzi huu. Huyu mgombea anamuunga mkono Maalim Seif, lakini upande wa pili [wa Profesa Lipumba] ulipoona anakubalika sana Liwale wakamchukua, nasi tukaona hatuna budi kumuunga mkono,” Mwananchi inamkariri Bungala.
Aliongeza kuwa wanafanya maandalizi kuhakikisha Maalim Seif anawasili Liwale na kufunga kampeni za mgombea huyo.
Hata hivyo, Sakaya amesema kuwa hawatakubali kuona Maalim Seif anakuja kushiriki kampeni hizo na kwamba atashughulikiwa na nguvu ya wananchi wenye katiba yao.
“Endapo akienda atakutana na nguvu ya Katiba ya CUF yaani wananchi na kitakachowapata wasishangae. Kama wao wanatumia nguvu kubwa kukibomoa sisi tunatumia Katiba,” alisema Sakaya.
Alisisitiza kuwa kambi ya Maalim Seif haina dhamira nzuri katika hatua hiyo, hivyo hawatakubaliwa kushiriki.
Uchaguzi wa Liwale utafanyika Oktoba 13 na kampeni za mwisho zitashuhudiwa Oktoba 12 mwaka huu.
CUF imekuwa kwenye mgogoro wa kiutawala tangu Profesa Lipumba alipotangaza kurejea katika nafasi ya uenyekiti wa chama hicho miezi kadhaa baada ya kutangaza kujiuzulu wakati wa mchakato wa uchaguzi mkuu 2015.
Pande hizo mbili zinaendelea na mvutano mahakamani.