Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai ameeleza kushtushwa kupitishwa kwa sheria inayomtaka mkulima kulipa ushuru wa bidhaa wa asilimia mbili kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) wakati kamati ya bunge ya Bajeti ilikata.
Amesema hayo Bungeni Jijini Dodoma, ambapo amehoji Kamati ya Bunge ya Bajeti, wanawezaje kupitisha kitu kama hicho.
Hata hivyo, mwenyekiti wa kamati hiyo, Baran Sillo amesema walilikataa jambo hilo, na hata taarifa yao bungeni, walipinga mpango huo.
Akijibu swali la Mbunge wa Namtumbo (CCM), Vita Kawawa aliyetaka kujua kama ni kweli wakulima wa tumbaku watatozwa kodi hiyo, Naibu Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe amesema kwamba ni kweli bunge lilipitisha sheria ya ushuru wa bidhaa wa asilimia mbili kwenye mazao ya kilimo.
Waziri Bashe amesema kuwa wizara haijaanza kukata ushuru huo kwa sababu mjengeko wa bei ya tumbaku huamuliwa kati ya Februari na Aprili, na kwamba wakati sheria inapitishwa, bei ilikuwa imepangwa.
Aidha amesema wamewasiliana na wizara ya fedha kuona namna wanavyoweza kutekeleza sheria hiyo ili kulinda maslahi ya wakulima.