Serikali kupitia Wizara Ya Habari, Utamaduni, Sanaa Na Michezo imetishia kuvifungia vyombo viwili vya kusimamia mchezo wa Ngumi PST na TPBO kwa kile kinachoelezwa kuwa wanaihujumu kamati mpya ya kusimamia masumbwi nchini.
Katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika Jijini Dar es Salaam Waziri wa Michezo Dkt. Harrison Mwakyembe ameelezea kukerwa kwake na watendaji wa vyombo hivyo huku akitoa onyo la mwisho kuwa wakiendelea na tabia hiyo atavifungia maisha.
Hatua hiyo ya Mwayembe imekuja baada ya mwenyekiti wa muda wa kamati ya kuboresha rasimu ya katiba ya ngumi za kulipwa kumuelezea vyama vinavyoleta vurugu kwenye ngumi ikiwa ni pamoja na kuidharau serikali kwa maagizo waliyopewa.
Mwenyekiti wa kamati wa muda ya maboresho ya katiba Emmanuel Saleh ameeleza kwa masikitiko kuwa vyama vya ngumi havitoi ushirikiano na kudharau mamlaka ya serikali.
Kutokana na kauli ya waziri Mwakyembe mmoja kati ya mabondia wa ngumi za kulipwa nchini Dullah Mbabe amefurahishwa na kauli ya waziri akieleza kuwa uamuzi huo una dhamira ya kusaidia mchezo wa ngumi.
TPBO inamilikiwa na Yassin Abdallah Ustadhi wakati PST inasimamiwa na Emmanuel Mlundwa.