Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, Amos Makalla leo amefanya kikao kazi na watendaji wa taasisi mbalimbali za Serikali zilizopo Dar es salaam, ikiwemo DAWASA, TRA, TANESCO, TANROAD, TARURA na DMDP ambapo ametaka kila taasisi kutekeleza wajibu wake ili kuondoa kero kwa wananchi.
Akizungumza wakati wa kikao hicho, RC Makalla amewapongeza TRA kwa kuvuka lengo la ukusanyaji wa Mapato kwa Mwezi huu na kuwaelekeza kuendelea kukusanya mapato kwa mujibu wa Sheria pasipo kuwabugudhi wananchi huku akisisitiza utoaji wa elimu kwa walipa Kodi.
Aidha, amewataka TANROAD na TARURA kuhakikisha wanafanya ukaguzi wa Mara kwa Mara kwenye Barabara zao na kufanyia ukarabati sehemu zenye changamoto ili kuondokana na kero ya ubovu wa barabara.
Amewataka kusimamia ipasavyo miradi ya Barabara huku akielekeza DMDP kushirikiana na Halmashauri kuweka miundombinu bora na kuhakikisha masoko yote yaliyojengwa yanaanza kutumika baada ya kubaini masoko mengi yaliyojengwa yamekosa wapangaji.
Pamoja na hayo RC Makalla amewaelekeza TANESCO kuhakikisha inafanyia kazi changamoto ndogondogo zinazowakabili ikiwa ni pamoja na kutoa taarifa mapema kwa wananchi pindi inapotokea matengenezo au hitilafu ili watu wajiandae.