Mradi wa Ujenzi wa Vituo vya Kupoza Umeme katika kila wilaya nchini unakadiriwa kutumia jumla ya shilingi trilioni 4.20 ambazo zitatolewa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Akiwasilisha Hotuba ya Bajeti ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati kwa Mwaka wa Fedha 2023/24 bungeni jijini Dodoma, January Makamba alisema kuwa mradi wa ujenzi wa vituo vya kupoza umeme vya Gridi ya Taifa unalenga kupunguza upotevu wa umeme unaotokana na umbali mrefu wa njia za usambazaji umeme katika maeneo mbalimbali nchini.
“Mradi huu umepangwa kutekelezwa katika awamu tano ambapo katika kila awamu vitajengwa vituo 15 vya kupoza umeme. Vilevile, Serikali kupitia TANESCO itaanza utekelezaji wa mradi huu kwa kufanya upembuzi yakinifu wa mradi, tathmini ya athari kwa mazingira na jamii, tathmini ya mali za wananchi watakaopisha mradi, kuanza taratibu za kuwapata Wakandarasi na kutafuta fedha za ujenzi wa mradi”, alisema Makamba.
Ameongeza kuwa, Serikali kupitia TANESCO imetenga shilingi bilioni 5.4 kwa ajili ya utekelezaji wa kazi hizo zilizopangwa kufanyika kwa mwaka wa fedha 2023/24.
Aidha, amefafanua kuwa, Wizara itaendelea kutekeleza vipaumbele ilivyojiwekea mwaka jana ikiwa ni pamoja na kuimarisha uzalishaji, usafirishaji na usambazaji wa umeme, kuimarisha upatikanaji wa nishati vijijini na vitongojini, kuendeleza shughuli za mafuta na gesi nchini pamoja na kuwezesha upatikanaji wa nishati safi ya kupikia.
Aidha, mkazo utaelekezwa katika kuimarisha utoaji wa huduma kupitia Taasisi zilizo chini ya Wizara, kushirikisha Sekta Binafsi katika uendelezaji wa Sekta ya Nishati pamoja na ushiriki wa wazawa katika shughuli za mafuta na gesi asilia.