Rais wa Marekani, Donald Trump amekana kuzitolea nchi za Afrika lugha chafu katika kikao kilichofanyika Ikulu, kuhusu sera ya uhamiaji ya DACA.
Trump alinukuliwa akitoa lugha ya matusi kwa nchi za Afrika akihoji kwanini wanawahitaji Waafrika nchini kwao na kwamba ni bora wangeruhusu zaidi watu kutoka Norway.
“Kwanini tunataka watu hawa wote kutoka Afrika waingie hapa? Ni watu kutoka nchi chafu (sh*thole countries)… tungekuwa na watu wengi zaidi kutoka Norway,” tafsiri isiyo rasmi ya nukuu ya Trump.
Hata hivyo, Trump ametumia mtandao wa Twitter ambako alishambuliwa vikali, kujitetea kuwa hakutamka maneno hayo kwenye kikao hicho ingawa amekiri kutumia maneno makali.
“Maneno niliyotumia kwenye kikao cha DACA yalikuwa magumu, lakini hiyo sio lugha niliyoitumia. Kilichokuwa kigumu zaidi kutoka kwangu ni kukataa pendekezo la kuirusha sera ya DACA,” tafsiri ya tweet ya Trump.
- Trump akerwa na Waafrika, awatolea lugha chafu
- Tatizo la rushwa ya ngono vyuoni kushughulikiwa vikali
DACA ni sera ambayo inawalinda vijana wadogo kupata nafuu katika taratibu za uhamiaji nchini Marekani, na kuwalinda zaidi kutofukuzwa kirahisi. Trump aliiondoa sera hiyo mwaka jana.
Mtandao wa Twitter uligeuka kaa la moto kwa Trump baada ya habari hiyo kuripotiwa na hasa watu kutoka Afrika ambao walianzisha hashtag na kujaribu kumuonesha uzuri wa Afrika.