Jaji wa jimbo la New York ameamuru Rais Donald Trump kuzirudisha dola milioni mbili alizozichukua kwa matumizi yanayotajwa na mahakama kuwa ni kinyume cha sheria.
Fedha hizo ni kutoka mfuko wa misaada wa ‘Trump Foundation’, ambapo inadaiwa alizichukua na kuzitumia katika kampeni zake kwenye uchaguzi wa mwaka 2016 uliomuingiza madarakani
Uamuzi huo umetokana mashitaka yaliyowasilishwa na ofisi ya mwanasheria mkuu wa Jimbo la New York dhidi ya mfuko wa misaada wa ‘Donald J Trump Foundation’ akiwemo Rais mwenyewe na watoto wake watatu Donald Junior, Ivanka na Eric.
Mahakama pia imeelekeza watoto wa rais Trump wanaosimamia uendeshaji wa mfuko huo wanatakiwa kupatiwa mafunzo ya uongozi na kujua namna ya kufanya maamuzi ya matumizi ya fedha kwa misingi inayokubalika kisheria.
“Donald Trump Jr, Eric Trump na Ivanka Trump – ambao pia walikuwa wakurugenzi wa Trump Foundation – wanapaswa kupata mafunzo ya lazima kuhusu majukumu ya kuwa watendaji na wakurugenzi wa mifuko ya misaada”, Alisema mwanasheria mkuu wa New York Letitia James.
Kutokana na uamuzi huo wa mahakama, Rais Trump ametakiwa kukiri waziwazi juu ya matumizi mabaya ya fedha za mfuko huo na kueleza kwamba wakati mwingine atazingatia masharti ya matumizi ya fedha za mfuko.