Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Simba SC Salim Abdallah ‘Try Again’ ameendelea kuwasihi Mashabiki na Wanachama wa klabu huiyo kuwa wastahamilivu katika kipindi hiki ambacho timu yao imeachwa kwa tofauti ya alama 10 dhidi ya Young Africans inayoongoza msimamo wa Ligi Kuu kwa sasa.
Try Again ametoa rai hiyo baada ya Young Africans kuibanjua Polisi Tanzania bao 1-0 jana Jumapili ‘Januari 23’ mjini Arusha kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, huku SImba SC ikiambulia sare ya bila kufungana dhidi ya Mtibwa Sugar Jumamosi ‘Januari 22’ na kufikisha alama 25.
Ushindi huo umeendelea kuiwezesha Young Africans kubaki kileleni ikiwa timu pekee ambayo haijapoteza mchezo katika Ligi Kuu tangu msimu huu 2021/22 ulipoanza.
Try Again amesema, mbio za ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu bado mbichi na wale wanaoichukulia poa Simba SC wajiandae kushangazwa mwishoni.
Try Again amesema kipigo cha Mbeya City kilichowafanya wateme alama tatu kwa mara ya kwanza msimu huu, kimewazindua na sasa kila mchezo kikosi chao kitacheza kwa tahadhari kubwa ili wasipoteze malengo yao ya kutetea ubingwa kwa mara ya tano mfululizo.
“Kila timu bado ina nafasi ya kuchukua ubingwa msimu huu, hata Simba tumo kama watetezi na tumejipanga ili kuhakikisha tunabeba tena, achana na hao wanaojidanganya, misimu iliyopita kuna timu ziliongoza msimamo, ila sisi tulimaliza mabingwa,” amesema Try Again na kuongeza
“Tumejipanga kuhakikisha hatupotezi ovyo pointi katika mechi zetu, ili kutimiza malengo, tunaamini kikosi tulichonacho tutatetea tena Inshallah.”
Simba SC kwa sasa inashikilia ubingwa kwa misimu minne mfululizo tangu 2018 na kama itabeba tena msimu huu itaandika rekodi ya kuwa timu ya kwanza kutwaa taji la Ligi Kuu mara mbili kwa misimu mitano mfululizo.
Awali Young Africans iliandika rekodi kwa kulibeba taji kwa idadi hiyo kati ya 1968-72 kisha Simba kujibu mapigo ikibeba mwaka 1976-80 na haijawahi kutokea tena timu yoyote kurudia rekodi hiyo, japo Simba kwa sasa ipo pazuri kuirudia tena.