Katibu Mkuu wa Shirika la Vyama vya Wafanyakazi Nchini (TUCTA) Henry Mkunda amemkumbusha Rais Samia ahadi yake ya kuboresha mishahara kwa wafanyakazi na kupendekeza kima cha chini cha mshahara kwa sekta zote kiwe Sh1, 010,000 milioni.
Mkunda ameyasema hayo leo Jumapili Mei Mosi, 2022 wakati akizungumza katika sherehe za siku ya wafanyakazi duniani inayofanyika katika uwanja wa Jamuhuri jijini hapa.
“Tunakumbuka ahadi yako ya kuboresha mishahara katika mwaka huu wa 2022, hivyo Tucta
tunapendekeza kiwango cha kumwezesha mfanyakazi kuishi kiwe walau Sh1, 010,000 kwa mwezi baada ya hizi tafiti kufanyika. Tutashukuru sana Mama kama utaliona hilo,”amesema.
Mkunda amesema sababu iliyowasukuma kuandaa kauli mbiu ya Mei Mosi ya mishahara na maslahi kwa wafanyakazi ndio kilio chetu, Kazi iendelee ni wafanyakazi kuwa raslimali na nyenzo ya kuinua uchumi katika nchi.
Amesema tafiti zinaonyesha kuwa mishahara na maslahi humwezesha mfanyakazi kufanya kazi kwa ubora na ufanisi na weledi.
Ameeleza kwa hivi sasa mshahara wa kima cha chini kwa sekta binafsi ni Sh40,000 na Sh60,00 kwa mfanyakazi wa majumbani wakati kwa wafanyakazi wa mashambani na viwandani ni Sh100,000 , viwango vilivyotangazwa mwaka 2013 katika gazeti la Serikali.
Amesema kwa upande wa umma, kima cha chini cha mishahara ni Sh300,000 kilichotangazwa mwaka 2015.
Mkunda amesema kufuatia hilo Tucta ilifanya utafiti mwaka 2006 na kuwasilisha mapendekezo Serikalini mapendekezo kuwa kima cha chini cha mshahara kinachomwezesha mfanyakazi kumudu mahitaji muhimu kwa wakati huo Sh315,000.
Amesema utafiti mwingine ulifanyika mwaka 2014 na kubaini kuwa malipo ya mshahara ya Sh720,000 kwa mwezi yangemwezesha mfanyakazi wa kima cha chini kumudu gharama za maisha.
Amesema pamoja na mapendekezo hayo viwango hivyo havijakubaliwa na Serikali na kwamba kutokubaliwa kwa mapendekezo hayo kumeathiri wafanyakazi na familia zao kutokana kupanda kwa gharama za maisha na kuwafanya kuishi maisha ya chini ya mstari wa umasikini.
Amesema pamoja na Uviko-19 na Vita vya Ukraine na Urusi bado wafanyakazi wanaomba kuweka kiwango kitaifa cha kima cha chini cha mshahara ili kuwezesha wafanyakazi kuishi.