Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo. Mhe, Mohamed Mchengerwa amezipongeza timu za Simba na Young Africans kwa kuonyesha kiwango kizuri katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara jana Jumamosi (April 30) Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Waziri Mchengerwa ametoa pongezi hizo leo Jumapili (Mei Mosi), huku kuwataka wachezaji kuwa na nidhamu wakiwa uwanjani ili timu ziweze kufika mbali kwenye mashindano ya kimataifa.

Mchengerwa ambaye alikuwa Mgeni Rasmi kwenye mchezo huo amesema kiwango kilichoonyeshwa na timu zote mbili, kimetia matumaini kuwa soka la Tanzania limeendelea kukua kutokana na timu zote kuonyesha ushindani mkubwa kimchezo.

Amesema mkakati wa Serikali kwa sasa ni kuendelea kuweka mazingira wezeshi na kuboresha miundombinu ya michezo ili Tanzania iweze kufanya vizuri.

Ameongeza kuwa kwa sasa Serikali imeendelea kugharimia kuziweka kambini timu zote za taifa zinazoendelea kufanya mazoezi kwa ajili ya mashindano ya kimataifa.

“Nisisitize tu kuwa Serikali kwa sasa imeshatenga fedha nyingi kuziwezesha timu zote za michezo mbalimbali ili zifanye vizuri zaidi na kupeperusha bendera ya taifa letu kwenye mashindano ya kimataifa”. Ameongeza Mhe, Mchengerwa

Aidha, amesema katika kipindi hiki Serikali inakwenda kusaka vipaji vya wanamichezo kupitia program ya ligi ya mama Samia ya Mtaa kwa mtaa.

Mchezo wa jana ulihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali na michezo na mashabiki ambao walifurika kwenye uwanja wa Benjamin Mkapa ambapo timu zote hazikufungana.

Baadhi ya viongozi waliohudhuria mechi hiyo ni pamoja na Waziri wa TAMISEMI. Mhe, Innocent Bashungwa, Mawaziri kutoka Tanzania Visiwani, Naibu Spika na Mbunge wa Ilala, Mhe. Musa Zungu, Mkurugenzi wa Michezo Yusufu Singo na wadau mbalimbali.

TUCTA yamkumbusha Rais Samia ahadi yake
Kocha Pablo: Tulibahatisha kumchezesha Chama, Sakho