Mahakama Kuu nchini Kenya, imesimamisha kwa muda Tume ya uchunguzi iliyoteuliwa na Rais wa Kenya, William Ruto kutafuta ukweli kuhusu mauaji ya watu na uhalifu mwengine katika msitu wa Shakahola.
Hatua hiyo, inafuatia Muungano wa Azimio la Umoja kwanza kufika Mahakamani na kumshtaki Rais Ruto wakidai amekiuka sheria katika uundaji wa tume hiyo, ambayo ilikuwa ikichunguza mauaji tata ya Mchungaji Paul Mackenzie, aliyewataka waumini wake wafunge hadi kufa ili wakakutane na Mungu.
Aidha, wakati hayo yakiendelea, Vyombo vya usalama nchini humo vinaripoti kuwa, mabaki ya mifupa ya watu 2 waliofariki imepatikana katika msitu huo wa Shakahola wakati zoezi la kutafuta miili likiendelea.
Mratibu wa eneo la Pwani, Rhoda Onyancha, anasema wanaendelea na kutafuta manusura na maiti katika msitu huo na hadi kufikia sasa watu waliopatikana wakiwa wamefariki msituni humo imefika 240.