Mbunge wa Singida Mashariki na Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu amekamatwa uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere International (JNIA) akielekea Kigali Rwanda kuhudhuria kikao cha Halmashauri ya EALS kinachotarajia kuanza hapo kesho.
Kamanda wa Polisi wa Viwanda vya Ndege, Martin Ortieno amesema kuwa ni kweli Lissu ambaye pia ni Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika TLS amekamatwa na kupelekwa Makao Makuu ya Polisi.
Aidha, Kamanda huyo wa viwanja vya Ndege Tanzania hakutaka kueleza sababu ambazo zimesababisha kukamatwa kwa Lissu hali ambayo imemsababishia kuahirishwa kwa safari yake ya Kigali.
Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema amesema kuwa Mwanasheria huyo amekamatwa jioni hii huku sababu za kukamatwa kwake hazijawekwa bayana.
“Lissu amekamatwa na watu ambao walijitambulisha kuwa ni maofisa Polisi kutoka Kanda Maalum ya Dar es salaam lakini hawakuweza kumueleza kosa lake ni lipi hivyo wakaondoka nae kutoka uwanja wa ndege,”amesema Mrema