Baada ya Mwanasheria Mkuu wa Chadema kukaa kwa muda wa saa nne ndani ya ukumbi wa Mahakama ya Wilaya ya Dodoma Mjini akihofia kukamatwa na Jeshi la Polisi Mkoani humo limekana kuwa na mpango huo.

Lissu alifika Mahakamani hapo mapema hii leo asubuhi kwaajili ya kusimamia kesi ya migogoro ndani ya Chama cha Walimu Tanzania (CWT) iliyokuwa ikisikilizwa na Hakimu, Proches Mushi.

Aidha, katika kesi hiyo, Kamati ya Utendaji ya (CWT) imefungua kesi dhidi ya Katibu Mkuu wa CWT, Yahaya Msulwa wakimtuhumu kwa matumizi mabaya ya madaraka na kwenda kinyume na katiba ya chama chao.

Wakati wakijadili muda wa kurudiwa tena kwa kesi hiyo mahakamani hapo, Lissu alisikika akisema kuwa kuna taarifa amezipata kuwa kuna polisi wamevalia kiraia wanamngojea nje ya ukumbi wa mahakama hiyo ili wamkamate na kumsafirisha kwenda Dar es salaam.

“Nimepewa taarifa kuwa hapo nje kuna polisi wananisubiri nikitoka wanikamate na kunisafirisha Dar es salaam kwa hiyo huenda hiyo (Julai 23) iliyopangwa kusomwa kwa kesi hii huenda nisiwe huru kuhudhuria kesi, nakaa humu ndani ya ukumbi wa mahakama ili nione kama watavunja sheria kuja kunikamata mahakamani, nilishazoea kukamatwa,”amesema Lissu

Hata hivyo, baada ya kukaa masaa manne mahakamani hapo, alifika Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Lazaro Mambosasa na kumweleza Lissu kwamba Jeshi la Polisi Mkoa wa Dodoma halina taarifa yoyote wala mpango wa kumkamata, na kuongeza kuwa kama wangekuwa na maelekezo ya kufanya hivyo wangekuwa tayari wameshamkamata, hivyo mara baada ya kuondoka Mambosasa, Lissu naye aliondoka mahakamani hapo.

Wahukumiwa kifo kwa kumdhalilisha mwanamke
Ryan Giggs Atia Shaka Usajili Wa Ivan Perisic