Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ridhiwani Kikwete amewahakikishia Wajumbe wa Kamati ya Kusimamia Ofisi za Viongozi Wakuu wa Kitaifa ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar kuwa Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa ipo tayari kushirikiana na Ofisi ya Nyaraka Zanzibar, ili kuhakikisha Ofisi hiyo inaboreshwa kwa maslahi mapana ya pande zote mbili za Muungano.
Kikwete ametoa kauli hiyo hii leo Desemba 13, 2023 wakati akizungumza na Wajumbe wa Kamati hiyo mara baada ya kutembelea Ofisi ya Rais, Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa, Kanda ya Mashariki iliyopo Jijini Dar es Salaam kwa lengo la kujifunza na kubadilishana uzoefu wa namna ya kutunza na kuhifadhi nyaraka na kumbukumbu za Taifa.
Amesema, Taifa lolote lisilo na Kumbukumbu ni Taifa lililokosa mwelekeo kwani halijui limetoka wapi na linaelekea wapi na kwamba kuiahidi Kamati hiyo kuwa Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa itatoa ushirikiano wa kutosha ili kuhakikisha kumbukumbu na Nyaraka za Viongozi Wakuu wa Zanzibar zinatunzwa na kuhifadhiwa kwa maslahi mapana ya Taifa.
Kwa upande wake Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Ikulu, Jamal Kassim Ali ameitaka ofisi ya Rais Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka kuunga mkono jitihada mbalimbali ili kuhakikisha kuwa Ofisi ya Nyaraka Zanzibar inaboreshwa.