Tyson Fury amefanikiwa kumpiga mpinzani wake Deontay Wilder kwenye pambano lao la marudiano lililomalizika muda mfupi uliopita, leo, Februari 23, 2020 akimpa tabu na kusababisha mwamuzi kumaliza pambano katika raundi ya saba (TKO).
Fury, maarufu pia kwa jina la ‘The Gypsy King’ amekuwa Bingwa wa Masumbwi ya Uzito wa Juu wa Dunia wa WBC, na kuweka rekodi ya kuwa bondia namba moja kwa sasa kwenye uzito huo asiye na rekodi ya kupigwa kwenye mapambano yake yote, akiwa na sare moja ya pambano la kwanza dhidi ya Wilder.
Hakuna aliyetarajia kuwa Fury angeweza kushinda pambano hilo kwa KO, wengi walitabiri kuwa Wilder angeshinda kwa KO au Fury angeshinda kwa alama baada ya kengele ya raundi ya 12.
Aidha, Fury ameweka rekodi ya aina yake kwa kuwa bondia wa kwanza kumuonjesha joto la kipigo cha TKO Wilder ambaye mapambano yake yote ameshinda kwa KO isipokuwa pambano lao la kwanza mbalo lilimalizika kwa sare.
Katika pambano la leo, Fury alimtesa Wilder akimpasua sikio lake na kusababisha damu nyingi kutoka huku watu wakisubiri mwamuzi tu amalize pambano.
Tangu raundi ya kwanza Fury alianza kwa kasi na kumpa presha kubwa Wilder ambayo ilimshinda kuhimili. Katika raundi ya 3, Fury alimpiga chini Wilder kwa mfululizo wa makonde mawili.
Fury ambaye ni bondia kutoka nchini Uingereza sasa ndiye mwenye nafasi ya kupambana na bondia mwenzake muingereza, Anthony Joshua.
Joshua naye alishachafua rekodi yake baada ya kupigwa kwa KO katika pambano lake la kwanza na Andy Ruiz Jr., ingawa alishinda tena kwa alama kwenye pambano lao la marudiano.
Kwa mara ya kwanza, Wilder alionja joto la kupigwa na kuanguka ulingoni, ingawa mwamuzi alimkata alama Fury kwa kurusha konde wakati ameamua mapumziko (break).