Kikosi cha Timu ya Taifa Chini ya Umri wa miaka 23, kimewasili salama nchini Nigeria, kwa ajili ya mchezo wa kuwania kufuzu Fainali za Mataifa ya Afrika (U23AFCON), zitakazounguruma mapema mwaka 2023 nchini Morocco.
Kikosi hicho kililazimissha sare ya 1-1 katika mchezo wa Mkondo wa Kwanza uliochezwa Uwanja wa Benjamin Mkapa Jumamosi (Oktoba 22), hivyo kitalazimika kusaka ushindi wa aina yoyote, au sare kuanzia 2-2, ili kutinga hatua inayofuata.
Mchezo huo umepangwa kuchezwa keshokutwa Jumamosi (Oktoba 29).
Kocha Mkuu Kikosi hicho Hemed Morocco amesema wapo tayari kwa mchezo wa Mkondo wa Pili ambao anaamini utakua mgumu sana, tofauti na ule wa Mkondo wa Kwanza.
“Tumewasili salama hapa Nigeria, tuna matumaini makubwa ya kufanya vizuri, naamini mchezo hautakua rahisi kwa sababu wenyeji wetu watahitaji kucheza kwa nguvu zote ili wafuzu wakiwa kwao.”
“Tumejiandaa kwa kila kitu, mapungufu yaliyojitokeza katika mchezo wa Mkondo wa Kwanza tumeyafanyia kazi na hilo linaniaminisha mambo yatakuwa mazuri ndani ya dakika 90 za mchezo wetu hapa Nigeria.”
Mshindi wa jumla wa mchezo huo atacheza na Uganda katika hatua ya mwisho kusaka nafasi ya kufuzu Fainali za Afrika chini ya Umri wa Miaka 23 (U23AFCON), zitakazounguruma Machi 20-28 mwakani, huku mshindi wa kwanza, pili na watatu watafuzu kucheza Michezo ya Olimpiki 2024.