Tume ya uchaguzi Nchini Uganda imepiga marufuku wapiga kura kwenda na simu na kamera kwenye kituo cha kupiga kura katika uhaguzi mkuu wa nchi hiyo utakaofanyika wiki ijayo Januari 14, na kutokubaki kituoni kusubiri matokeo.
Agizo hilo limetolewa na Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Uganda Jaji Simon Byabakama Mjini Kampala huku mashirika yasiyo ya s erikali yakitaka tume kufafanua kuhusu teknolojia itakayotumiwa katika Uchaguzi huo zikiwa zimesalia siku saba kufanyika zoezi hilo.
Mwenyekiti huyo ametangaza kanuni zitakazotumiwa katika uchaguzi huo, ikiwa ni pamoja na kupiga marufuku waandishi habari kuingia ndani kwenye vituo vya kupiga kura na kuvaa sare za chama chochote cha siasa.
Aidha, Jaji Simon ameongeza kuwa wapiga kura wakibaki kwenye vituo vya kupiga kura watasababisha msongamano mkubwa wa watu na kuvunja kanuni za watalaam wa afya za kudhibiti virusi vya corona.