Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto (Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii) chini ya uratibu wa Kamishina wa Ustawi wa Jamii imeunda timu maalum ya wataalam wa Ustawi na Maendeleo ya Jamii kwa ajili ya kufanya tathmini ya athari na mahitaji yanayotokana na janga la moto mkoani Morogoro pamoja na kutoa huduma ya msaada wa Kisaikolojia.
Hayo yamesemwa mkoani Morogoro na Kamishna wa Ustawi wa Jamii Dkt. Naftali Ng’ondi wakati alipofika katika maeneo mbalimbali kuzungumza na ndugu, jamaa na marafiki waliopoteza wapendwa wao katika ajali hiyo.
Kamishna Ng’ondi amesema kuwa katika zoezi hilo Wizara inashirikiana na wataalam kutoka ngazi ya Mkoa, Halmashauri na wataalam kutoka Chama cha wataalam wa Ustawi wa Jamii (TASWO), Taasisi ya Ustawi wa Jamii na Chuo Kikuu cha Dar es salaam.
Amezitaja huduma zitakazotolewa na wataalam hao kuwa ni kutoa huduma ya Msaada wa Kisaikolojia na kijamii kwa watoa huduma Hospitalini, kuzuia matatizo zaidi ya kimwili, Kiroho na kiakili, na kujumuisha hatua za matibabu kwa waathirika, ikiwa ni pamoja na aina mbalimbali za ushauri, kama vile ushauri wa huzuni (Bereavement Counseling) baada ya ajali na kuunganisha wagonjwa kwa wataalamu na vituo vya matibabu.
Kamishna Ng’ondi ameeleza kuwa Idara ya Ustawi wa Jamii na Maendeleo ya jamii zitasaidia pia kuwaunganisha wahanga na programu za kijamii (Wahudumu wa Mashauri ya Kijamii – Community Case Workers, Para Social Workers) zitakazowasaidia watoto kuondokana na hali ya majonzi na kuwaunganisha na huduma za kijamii kulingana na mahitaji na upatikanaji wa huduma na rasilimali zilizopo zikiwemo Hospitali, Mamlaka za Serikali za Mitaa, Asasi za kiraia na watoa huduma binafsi.
Aidha, Wizara kwa kushirikiana na wataalam kutoka Mkoa wa Morogoro wanaandaa jumbe mbalimbali kwa ajili ya kuelimisha jamii kuhusu ulinzi na usalama kwa jamii na jinsi ya kukabiliana na majanga ili kuepukana na majanga yanayoweza kuepukika.
Ajali ya Lori la mafuta lililolipuka eneo la Msamvu mjini Morogoro, Jumamosi tarehe 10/08/2019 saa mbili asubuhi limesababisha vifo zaidi ya watu 76 na majeruhi zaidi ya 40 waliungua kwa moto baada ya lori lililokuwa na shehena ya mafuta kupata ajali na kisha kupinduka na kulipuka moto.