Naibu Waziri Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Abdalah Ulega amesema kuwa Serikali ina mpango wa kuifanya sekta ya Mifugo na Uvuvi kuwa na mchango mkubwa katika pato la Taifa.
Ameyasema hayo Mkoani Kigoma alipokuwa katika ziara ambayo alikuwa ameambatana na kamati ya kudumu ya Bunge ya Kilimo Mifugo na Maji kutembelea  chuo cha wakala wa Elimu na Mafunzo ya Uvuvi (FETA)  kampasi ya kigoma.

Amesema kuwa Wizara ina Mkakati  wa kulinda rasilimali za Mifugo na Uvuvi, kwa kuimarisha uvuvi wa bahari kuu na kuitoa sekta hiyo kwenye kuchangia kiasi na shilingi Bilioni 19 kwa mwaka katika pato la taifa hadi kufikia kuchangia zaidi ya shilingi Bilioni 50 kwa mwaka.

“Tunaweza kufikia malengo haya kwanza kwa kuimarisha uvuvi wa Bahari kuu kwa kuhakikisha kwanza taasisi yetu ya kusimamia uvuvi wa bahari kuu inakuwa na nguvu kwa kuweka vizuri sheria na kanuni zetu za uvuvi ikiwa ni pamoja na kufufua shirika letu la TAFICO, amesema Ulega.”

Aidha, amesema kuwa Serikali ina mkakati wa kuwa na Meli ambayo itakuwa na uwezo wa kwenda kuvua na kuchakata mazao ya samaki, jambo ambalo litakwenda sambamba na ufunguaji wa viwanda vya uchakataji wa mazao ya uvuvi.

 

Hata hivyo, kwa Upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi kutoka Sekta ya Uvuvi, Dkt. Yohana Budeba amesema kuwa njia ya ufugaji wa samaki wa kisasa kupitia chuo cha FETA kitatengeneza wataalam na kuongeza ajira na kupatikana samaki wengi na kupelekea mchango mkubwa wa sekta ya uvuvi katika uchumi wa taifa hili.

Rais wa Mauritius ajiuzulu
Kamati ya kudumu ya Bunge kunusuru mto Ruaha