Kamati ya kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira imeendelea na ziara ya kazi kwa kupokea taarifa ya hali ya Mazingira Mkoani Iringa.

Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais, Kangi Lugola amesema kuwa ni vyema Kamati hiyo imetembelea Mkoa wa Iringa kwa  kuwa kuna changamoto kubwa ya kimazingira katika Mto Ruaha Mkuu na Ofisi yake iliunda kikosi kazi maalumu cha kunusuru mto huo.

“Naamini Kamati itaishauri Serikali kutenga fedha zaidi kwa ajili ya kuendeleza usimamizi wa mazingira nchini, maana maendeleo yoyote kwa namna moja ama nyingine yanategemea hifadhi endelevu ya mazingira” Lugola asisitiza.

Akitoa taarifa ya Mkoa wa Iringa mbele ya Kamati hiyo ya Bunge, Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza amesema kuwa Kamati hiyo ni muhimu sana kwa kuwa suala la Mazingira na Viwanda vinachangia katika ukuaji wa Uchumi kwa kuzingatia malengo ya Serikali ya kuwa na Uchumi wa Viwanda.

Amesema kuwa katika Mkoa wake kampeni ya Upandaji miti kama ilivyoelekezwa na Serikali  inatekelezwa ipasavyo kwakuwa kila Wilaya imevuka lengo la kupanda miti Milioni Moja na Laki tano kila mwaka, na kupelekea Mkoa kuwa chanzo kikubwa cha upatikanaji wa mbao na nguzo za umeme.

Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Viwanda, Biashara na Mazingira, Innocent Bashungwa ameupongeza uongozi wa Mkoa wa Iringa kwa kuwa mstari wa mbela katika kuhimiza suala la upandaji miti na kutoa wito kuwa kampeni hii ya upandaji miti kwa wingi ifanyike nchi nzima na kuitaka Ofisi ya Makamu wa Rais kupitia Mfuko wa Mazingira kusaidia rasilimali fedha kwa ajili ya kampeni hiyo.

Hata hivyo, Kamati hiyo inaendelea na ziara yake katika Mkoa wa Iringa ambapo itatembelea vyanzo mbali mbali vya maji vilivyohifadhiwa katika Wilaya ya Iringa Vijijini.

Ulega kuibadiri sekta ya Mifugo na Uvuvi
Video: Mchungaji KKKT ahojiwa na Polisi, Mbunge Mtulia atoa hofu, asema yupo fiti