Polisi na wanajeshi wa ulinzi wa Taifa wamepelekwa katika majengo ya Bunge kuimarisha ulinzi kote nchini Marekani ikiwa ni maandalizi ya uwezekano wa kutokea wimbi la maandamano yenye vurugu ya wafuasi wa Rais Donald Trump.
Maafisa wa serikali kuu na za majimbo wameonya kuhusu uwezekano wa kutokea upya vurugu karibu na mabunge ya majimbo baada ya kundi kubwa la wafuasi wa Trump kuvamia jengo la Bunge la Marekani mjini Washington DC mnamo Januari 6.
Maandamano ya Januari 17, yalianza kwa njia ya utulivu na amani, katika mabunge ya Ohio, South Carolina, Texas na Michigan, ambapo baadhi ya waandamanaji waliripotiwa kuwa na silaha.
Wafuasi wa Trump wanaamini kuwa alishinda uchaguzi na kuwa uchakachuaji ulifanyika katika kiwango kikubwa, licha ya kutokuwepo kwa ushahidi wa kuridhisha mahakamani tuhuma hizo.
Sherehe ya kumuapisha Rais mteule Joe Biden itafanywa Jumatano Januari 20 ambapo taarifa zimesema sherehe hizo zitahudhuriwa na watu wachache.