Serikali kupitia Wizara ya Afya, imezindua Baraza jipya la Madaktari Tanganyika linalotarajia kudumu kwa muda wa miaka mitatu, huku moja ya jukumu la Baraza hilo ni kumshauri Waziri wa Afya katika masuala ya udhibiti, utoaji huduma na mafunzo kwa wataalamu wa Udaktari, Udaktari wa Meno na Afya Shirikishi.
Uzinduzi huo umefanyika katika ukumbi wa Jakaya Kikwete Jijini Dodoma na Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu, na kulohudhuriwa na Wakurugenzi wa Wizara, Wasajili wa Mabaraza, Wasajili wa bodi na Watumishi mbalimbali wa Wizara ya Afya.
Akizidua Baraza hilo, Waziri Ummy amelitaka kusimamia viapo na maadili ya taaluma zao yanavyoelekeza, hususan kwenye suala la kuokoa maisha ya mgonjwa kwanza kabla ya kutanguliza maslahi binafsi ikiwemo ya fedha jambo ambalo ni kinyume na viapo na maadili ya taaluma ya Udaktari.
Amesema Pamoja na kazi kubwa na nzuri iliyofanywa na Baraza lililomaliza muda wake, bado kuna kazi kubwa ya kufanya katika kusimamia Madaktari, huku akitaka kujua katika miaka mitatu ya Baraza ni madaktari wa ngapi wamechukuliwa hatua za kusimamishiwa sajili zao au kupewa onyo katika kipindi hicho.