Rais wa Baraza la Umoja wa Afrika, Musa Faki Muhammed, amezitaka pande zote nchini Sudan kufikia makubaliano ya kuweka serikali ya muda ya kiraia, ambayo itaongoza nchi hiyo kufanya uchaguzi katika hali ya uadilifu, haki na uwazi.
Muhammed ambaye alifanya ziara ya siku mbili nchini Sudan aliandaa taarifa yake aliyosema kwamba alipata kukutana na wajumbe wa baraza la kijeshi linaloongoza serikali ya mpito, pia alikutana na vyama vya kisiasa na makundi ya kijamii kufanya nao mkutano wa kiushauri.
Muhammed amewataka wadau wote nchini Sudan kuweka mbele maslahi mapana ya Sudan.
Hata hivyo viongozi wa maandamano ya wananchi nchini Sudan wamesema wamesimamisha mazungumzo na Baraza la Mpito la Kijeshi huku wakitoa wito kwa Wasudan kuendeleza maandamano nje ya makao makuu ya jeshi mjini Khartoum na miji mingine.
Msemaji wa harakati ya waandamanaji Mohamed al Amin alitangaza uamuzi huo wakati alipohutubia maelfu ya waandamanaji nje ya makao makuu ya jeshi hadi pale jeshi litakapotekeleza takwa lao la kutaka baraza la kiraia lishikilie madaraka kwa muda.
Wakati huo huo mapema jana Jumapili Mkuu wa Baraza la Mpito la Kijeshi Abdel Fattah al-Burhan alisema yuko tayari kuwakabidhi madaraka wananchi huku akisema atajibu matakwa yao katika kipindi cha wiki moja ijayo.