Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ameitaka mamlaka nchini Msumbiji kuchunguza ripoti kuwa wanamgambo wamewaua takribani watu 50 na kuwachinja wanawake na watoto katika mji wa Carbo del Gado Kaskazini mwa nchi hiyo.
Katika shambulio la hivi karibuni, wanamgambo wa Kiislamu waliubadili uwanja wa mpira wa miguu kuwa ‘’uwanja wa mauaji”, ambapo walikata vichwa na miili.
Matukio ya hivi karibuni ya kukata vichwa ni mfululizo wa mashambulizi yaliyotkelezwa na wanamgambo katika mji ulio na utajiri wa gesi Cabo Delgado tangu mwaka 2017.
Takriban watu 2,000 wameuawa na wengine 430,000 wameachwa bila makazi katika eneo hilo lenye mzozo linalokaliwa na idadi kubwa ya Waislamu.
Wanamgambo hao wanaohusishwa na kundi la Islamic State(IS),wanaonekana kuweka mizizi Kusini mwa Afrika.
Kundi hilo limetumia umaskini na ukosefu wa ajira kama kichocheo kuajiri vijana katika mapigano yao ya kuanzisha utawala wa Kiislamu katika eneo hilo.
Shirika la kutetea haki za binadamu Amnesty International limewatuhumu wanajeshi wa Msumbiji kwa kufanya ukatili wakati wa kudhibiti vurugu hizo, lakini wizara ya ulinzi imeonekana kutotilia maanani ripoti hizo.