Baraza la haki za binadamu la Umoja wa Mataifa limepiga kura ya kufanya uchunguzi wa kampeni yenye utata dhidi ya watuhumiwa wa madawa ya kulevya nchini Ufilipino inayoongozwa na rais Rodrigo Duterte.
Azimio hilo lililopendekezwa na Iceland, lilipitishwa na nchi 18 huku nchi 14 zikilipinga na nchi 15 zikiepuka kupiga kura ikiwemo Japan.
Idadi kamili ya vifo katika kampeni hiyo haiwezi kuthibitishwa, lakini kiasi cha watu 6,000 wanaaminika kuuawa tangu rais Duterte alipoanzisha kampeni baada ya kuingia madarakani mwaka 2016.
Asasi za kiraia zinasema idadi ya waliouawa ni kubwa, ikiwemo watuhumiwa wanaouawa na magenge ya watu wanaodaiwa kufadhiliwa na polisi.
Kwa upande wake, Shirika la Human Rights Watch limesema kuwa zaidi ya watu 12,000 wameuawa, ambapo Shirika la Amnesty International lilitoa rai kwa Umoja wa Mataifa kufanya uchunguzi juu ya uwezekano wa uhalifu dhidi ya ubinadamu.