Nchi ya Urusi imepigwa marufuku na Kamati ya Kimataifa ya Olympiki kushiriki mashindano yajayo ya Olympiki za michezo ya barafu inayotarajiwa kufanyika huko Pyeongchang.
Katazo hilo linakuja kufuatia uchunguzi wa madai ya mwaka 2014 wakati Urusi ilipoandaa michezo hiyo huko Sochi ambayo Urusi ilituhumiwa kufadhili dawa za kusisimua misuli michezoni ambazo zimepigwa marufuku duniani.
Hata hivyo Kamati hiyo imesema, kwa wachezaji wa Urusi ambao wanaamini na kuthibitisha kuwa wako safi wataruhusiwa kushiriki michezo hiyo itakayofanyika Korea Kusini, katika bendera isiyo na upande.
“Hili linachora mstari wa mwisho katika mfululizo wa matukio ya uharibifu,” walisema IOC.
Uamuzi huo umelaaniwa kila kona ya Urusi huku baadhi ya wabunge wakitaka kugomea michezo hiyo ingawa maafisa wengine wakipokea vema hatua ya kukaribishwa kwa wachezaji watakaokuwa wasafi kushiriki.
Rais wa IOC, Thomas Bach na bodi yake ambao walitoa tangazo hilo mjini Lausanne Jumanne –wamekuja na uamuzi huo baada ya kupokea taarifa na mapendekezo yalitokana na uchunguzi wa miezi 17 ulioongozwa na aliyekuwa rais wa Uswisi, Samuel Schmid.
Kamati ya OIympiki ya Urusi (ROC) iliondolewa kwenye ushiriki wa michuano hiyo lakini IOC imesema, itawaalika wanamichezo wasafi ikimaanisha wasiotumia dawa hizo za kusisimua misuli kushiriki michezo hiyo inayotarajiwa kufanyika Februari, mwakani chini ya mwamvuli wa jina ‘Wachezaji wa Olimpiki kutoka Urusi’ (OAR).