Urusi imemshambulia kwa maneno Rais wa Marekani, Joseph Biden kwa kauli yake aliyoitoa akimuita Rais wa nchi hiyo, Vladimir Putin ‘mhalifu wa kivita’.
Kauli hiyo ya Rais Biden inamuweka Rais Putin kwenye kundi moja na wahalifu wa kivita kama Joseph Kony anayeendeleza vita ya msituni dhidi ya Uganda, au Bosco Ntaganda wa DRC Congo ambaye alihukumiwa na Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai (ICC) kifungo cha miaka 30 jela na faini ya $30 milioni, baada ya kupatikana na hatia ya mauaji na ubakaji akiendesha vita haramu ya msituni.
Msemaji wa Kremlin – Urusi, Dmitry Peskov amewaambia waandishi wa habari kuwa kauli hiyo ya Biden haikubaliki na haisameheki.
Hata hivyo, Msemaji wa Ikulu ya Marekani, Jen Psaki alijibu kauli za Urusi akieleza kuwa Rais Biden alikuwa anajibu tu swali la moja kwa moja.
“Wote tumeona matendo ya kinyama ya dikteta wa nchi hiyo ambaye anatishia na kuchukua maisha ya raia, kushambulia hospitali, wanawake ambao ni wajawazito, waandishi wa habari na wengine,” amesema Jen Psaki.
Urusi imemuwekea vikwazo Rais Biden ikiwa ni pamoja na kumpiga marufuku kukanyaga ardhi ya nchi hiyo.