Serikali imesema utendaji kazi wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA,) unawapa nguvu ya kuwapa miradi mingine mingi ya maendeleo kutokana na ubora wa kazi inayofanyika pamoja na kurudisha kwa jamii fedha wanazozipata kupitia miradi wanayoisimamia.

Hayo yameelezwa na Mkuu wa Wilaya ya Ilala Arch. Ng’wilabuzu Ludigija wakati akizindua na kukabidhi majengo yaliyojengwa na kukarabatiwa na TBA katika shule ya Sekondari Juhudi iliyopo katika Kata ya Gongolamboto.


”Nitafikisha hili kwa Mh. Rais hasa hili la mchango wa TBA kwa jitihada hizi wanazoonesha pamoja na juhudi za walimu wa shule hii wanaojituma katika kuhakikisha kila mtoto wa kitanzania anapata elimu bora…..Tumeona ukarabati wa jengo la utawala, ujenzi wa matundu 20 ya vyoo na kubwa zaidi ni ujenzi wa ofisi ya Serikali ya wanafunzi ambayo itatumiwa na viongozi wa wanafunzi wa shule hii.” Amesema.


Mara baada ya kutembelea miradi hiyo yenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 43 amejiridhisha kwa ubora na viwango na kuwataka wanafunzi hao kutunza miundombinu hiyo.


”Kati ya shule 10 zinazofanya vizuri kiwilaya na hii ipo na ukarabati huu utaleta chachu  zaidi na matokeo yatakuwa bora zaidi….na TBA wamesema kwa awamu ya pili wataboresha  zaidi ofisi za walimu pamoja na miundombinu ya madarasa.” Amesema.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Idara ya Miliki Said Mndeme, amesema Aprili mwaka jana TBA ilialikwa kama mgeni rasmi katika mahafali ya kidato ha sita na kupitia risala iliyowasilishwa na wanafunzi wao wakaona ni vyema kushiriki katika kuboresha sekta hiyo muhimu.

”Katika kuunga jitihada za Serikali ya awamu ya sita katika kuboresha sekta ya elimu tukaona tushiriki ujenzi na ukarabati wa miundombinu na kwa awamu ya kwanza imekamilika.” Amesema.

Mndeme amesema, kwa awamu ya kwanza wamefanikiwa kujenga vyumba viwili vya ofisi ya Serikali ya wanafunzi, matundu ya vyoo 20, jengo la utawala na vimbweta na kwa awamu ya pili wataendelea na ukarabati wa madarasa kwa kuweka miundombinu ya umeme pamoja na kukarabati ofisi ya walimu.

Awali akitoa taarifa ya shule hiyo makamu mkuu wa shule hiyo Gasper Kagaruki amesema kuwa shule hiyo yenye kidato cha kwanza hadi sita ina wanafunzi wapatao 3000 imepokea miundombinu hiyo ambayo kwa sehemu kubwa itatua baadhi ya changamoto.

Amesema ujenzi wa matundu 20 ya vyoo imemaliza msongamano wa wanafunzi na ujenzi wa ofisi ya Serikali ya wanafunzi utawasaidia sana wanafunzi hao ambao viongozi wake wamekuwa wakitatua changamoto mbalimbali zinazowakabili wanafunzi wenzao na kufanikisha kupatikana na sare za shule na vifaa vya shule.

Pia ameishukuru wakala hiyo kwa kuonesha nia dhabiti ya kuboresha sera ya elimu na kuwaomba wadau wengine kujitokeza na kuboresha sekta hiyo muhimu.

Urusi yamshambulia Biden kwa kumfananisha Putin na Joseph Kony wa Uganda
Halmashauri zaaswa kusimamia miradi