Uongozi wa Geita Gold FC unahaha kuwabakisha nyota wawili wa timu hiyo msimu ujao, Mlinda Lango kutoka Burundi Arakaza MacArthur na mshambuliaji, Elias Maguri kutokana na mikataba ya mastaa hao kufikia ukomo msimu huu.
Mwenyekiti wa timu hiyo, Leonard Bugomola amesema mazungumzo baina yao na nyota hao yanaendelea ingawa kwa sasa akili zao wamezielekeza katika michezo hii ya mwisho ili wamalize vizuri.
“Tuko kwenye michezo ya mwisho ya msimu lakini tunaendelea kufanyia tathimini ya timu yetu kwa msimu ujao na kabla ya usajili wa nyota wapya tutaanza kwanza kuboresha mikataba ya wale wote ambao wanamaliza,” amesema.
Kwa upande wa Maguri akizungumzia juu ya hatima yake ndani ya timu hiyo alisema suala la kubaki au kuondoka itafahamika mwisho wa insimu huu.
“Siwezi kusema kama nitaondoka au nitabaki kwa sababu hakuna anayejua kesho yetu, najivunia kufanya kazi hapa kutokana na heshima niliyoipata tangu nimejiunga nao dirisha dogo la Januari mwaka huu,” amesema.
Maguri tangu ajiunge na kikosi hicho Januari mwaka huu amekuwa na kiwango kizuri kwani hadi sasa amefunga mabao matano ya Ligi Kuu Bara huku akiwahi kuzichezea timu mbalimbali zikiwemo Simba na Ruvu Shooting.
Kwa upande wa Arakaza, alijiunga na timu hiyo Julai mwaka jana akitokea Lusaka Dynamos ya nchini Zambia akiwahi pia kucheza Sports Club Villa ya Uganda, FC Dikhil ya Djibouti na Kakamega Homeboyz FC ya Kenya.
Timu nyingine alizozichezea nyota huyo ni Vital’O FC na Flambeau du Centre ambazo zote zinatoka Burundi.