Wakati Ligi Kuu ya Wanawake Tanzania Bara, ikitarajiwa kuanza Novemba 26, 2017 katika vituo viwili vya Dar es Salaam na Arusha, tayari usajili wa msimu kwa timu zote 12, umekamilika.
Kwa mujibu wa kalenda ya mashindano, usajili ulipangwa ufanyike kati ya Oktoba 25 na Novemba 12, mwaka huu na kwamba kuanzia leo Novemba 13 hadi 17, mwaka huu ni kipindi cha pingamizi.
Novemba 18, mwaka huu kutakuwa na kikao cha Kamati ya Sheria kabla ya Novemba 20, mwaka huu kutoa leseni za wachezaji.
Novemba 24, mwaka huu kutakuwa na Semina ya Viongozi wa klabu, Waamuzi na Makamishna jijini Dar es Salaam.
Ligi hatua ya makundi ikianza Novemba 26, mwaka huu ukomo utakuwa Desemba 9, mwaka huu Ligi Kuu na kupata jumla ya timu nane ambazo zitacheza ligi hatua ya Nane Bora ‘Super 8’ itaanza Desemba 20, mwaka huu. Ligi inatarajiwa kumalizika Machi 28, mwakani.
Timu zilizosajili kutoka Kundi A ambazo ziko Dar es Salaam ni Simba Queens ya jijini Dar es Salaam iliyopanda daraja msimu huu. Timu nyingine kwenye kundi hilo ni Mburahati Queens, JKT Queens, Evergreen zote za Dar es Salaam pamoja na timu za Fair Play ya Tanga na mabingwa watetezi – Mlandizi Queens.
Kundi B litakuwa na timu za Alliance ya Mwanza ambayo imepanda kutoka kituo cha Dodoma. Timu nyingine ni Marsh Academy pia ya Mwanza; Panama ya Iringa; Kigoma Sisterz ya Kigoma, Baobab ya Dodoma na Majengo Queens ya Singida.