Jeshi la Polisi mkoani Arusha, limepokea msaada wa pikipiki mbili zenye thamani ya shilingi milioni sita na laki moja toka Hoteli ya Kitalii ya Gran Melia iliyopo mkoani humo kwa lengo la kuunga mkono juhudi za Serikali za kuhakikisha watalii wanakua salama wakati wote.

Akipokea pikipiki hizo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, ACP Justine Masejo amesema pikipiki hizo ni msaada mkubwa wa kuhakikisha usalama katika mitaa mbalimbali hasa kwa watalii wanaofika mkoani hapo kwa kuzingatia Arusha ni kitovu cha utalii nchini.

Amesema, pikipiki hizo zitatumiwa na Askari wa kituo hicho cha Polisi cha Utalii na Diplomasia ambao walipewa mafunzo maalumu toka Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino ya namna bora ya kuwahudumia watalii na kuhakikisha usalama wao kupitia programu ya utalii salama.

Aidha ameongeza kuwa, jeshi hilo lilipokea jumla ya simu za mkononi 32 ambazo zilitolewa na Mbunge wa Arusha Mjini mheshimiwa Mrisho Gambo ambazo wamepewa viongozi wa vikundi vyote vya ulinzi shikirikishi katika jiji hilo maalumu kwa ajili ya kutoa taarifa dhidi ya uhalifu kwa jeshi la polisi.

Naye Meneja Msaidizi wa Hoteli hiyo, Vikram Singh amesema wametoa pikipiki hizo kuunga juhudi za Jeshi la Polisi kutokana na kazi kubwa wanayoifanya ya kuhakikisha Arusha inakua salama hususani kwa wageni wanaofika mkoani humo.

Rais Samia akutana na Sheikh Shakhboot wa UAE
Utoaji leseni bila utaratibu, wafanyakazi TRA mbaroni