Serikali inakusudia kupima utendaji wa Wakurugenzi na Wakuu wa Idara kwa kuangazia usimamizi wa mapato na makusanyo ya ndani, upelekaji wa fedha kwenye miradi ya maendeleo sambamba na uzuiaji na utekelezaji wa hoja za ukaguzi zinazoibuliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ameyasema hayo hii leo Juni 30, 2022 Bungeni jijini Dodoma, na kudai kuwa watendaji hao pia watapimwa kwa namna wanavyosimamia mikopo ya asilimia 10 ikiwa ni pamoja na marejesho, usimamizi wa miradi ya maendeleo.
“Serikali imejipanga vema kuendelea kusimamia suala la uwajibikaji katika utumishi wa umma kwa kuweka mikakati mbalimbali. “Mikakati ipo katika kuimarisha uwajibikaji hususan kwenye Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa ni pamoja na kupima utendaji wa utendaji wa Wakurugenzi na Wakuu wa Idara,” amesema.
Aidha, ameitaja mikakati mingine kuwa ni kongeza bajeti ya matumizi mengineyo katika Ofisi za Wakuu wa Mikoa na Wilaya kutoka shilingi bilioni 57.44 hadi shilingi bilioni 79.09 ili kuwezesha utekelezaji wa majukumu ya ofisi hizo.
“Serikali pia, imehuisha muundo wa Sekretarieti za Mikoa kwa kuboresha iliyokuwa Sehemu ya Usimamizi wa Serikali za Mitaa na kuwa Sehemu ya Menejimenti, Ufuatiliaji na Ukaguzi ili kuimarisha ufuatiliaji wa mapato, matumizi na utekelezaji wa miradi katika Mamlaka za Serikali za Mitaa.”
Waziri Mkuu ambaye alikuwa akitoa hoja ya kuahirisha Mkutano wa saba wa Bunge la 12 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, amesema hatua hiyo ni dhamira nzuri ya Rais Samia Suluhu Hassan, inayojiakisi kwenye Mpango na Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2022/2023.
Amesema, Serikali itaendelea kuwajengea uwezo Madiwani, Mafisa Tarafa na Watendaji wa Kata kupitia Programu ya Uimarishaji Tawala za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa lengo la kuongeza uelewa wa majukumu yao kisheria.
Hata hivyo, Waziri Mkuu amesema Serikali inaendelea kujenga mifumo na miundo wezeshi katika eneo la ufuatiliaji na tathmini ili kuboresha utendaji kazi unaojali matokeo na kudai kuwa uwepo wa mifumo na miundo imara ambayo itawezesha kujenga msingi thabiti wa usimamizi wa utendaji kazi wa Serikali ni suala la kuzingatia.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amesema Serikali imeanza maandalizi ya Sera ya Ufuatiliaji na Tathmini kwa kuzihusisha taasisi simamizi zinazohusika na ufuatiliaji na tathmini ili kuchambua maeneo wanayosimamia na kuhakikisha maeneo yote muhimu yanajumuishwa.
Amesema, Serikali imehuisha Muundo na Mgawanyo wa Majukumu wa Ofisi ya Waziri Mkuu hususan kwa upande wa Sera, Uratibu na Bunge ili kuimarisha jukumu la ufuatiliaji na tathmini kwa lengo la kuhakikisha taarifa za ufuatiliaji na tathmini kutoka katika wizara na taasisi za Serikali zinafanyiwa uchambuzi wa kina.
Waziri Mkuu, pia ametoa wito kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kushirikiana na Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Ofisi ya Waziri Mkuu na Wizara ya Fedha na Mipango kufanyia kazi changamoto ya uhaba wa wataalamu wa ufuatiliaji na kutathmini kazi za mifumo ya ukusanyaji wa taarifa yenye kuathiri ubora wa takwimu.