Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Iringa Mjini kupitia kwa Mwenyekiti wake, Silvastory Ngerera kimeaminika siri ya mkakati wa kumng’oa Mbunge wa Iringa Mjini (Chadema), Peter Msigwa kupitia uchaguzi mkuu ujao.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara ulioandaliwa na diwani wa Kata ya Kitanzini, Mahadhi Hepautwa, mwenyekiti huyo ameeleza kuwa amesikia Msigwa akijigamba kuwa chama hicho hakina mgombea wa kumuondoa katika nafasi hiyo kwenye uchaguzi ujao. Aliongeza kuwa amemsikia akieleza kuwa anazo siri zote za chama hicho kuhusu mkakati huo.
Hivyo, Ngerera alimtaka kutambua kuwa alichonacho sio siri bali ni taarifa tu, ndipo alipoamua kumpa kile alichokieleza kuwa ni siri asiyoijua.
“Msigwa anasema anapata siri nyingi za chama chetu, mwambieni kuwa hizo anazopata ni taarifa sio siri, ila leo hii nataka nimpe siri kubwa ambayo hajawahi kuipata, siri hiyo ni kuwa kwa mwaka 2020 CCM Iringa Mjini tumejipanga kwa udi na uvumba Msigwa ni lazima atoke mjini hapa,” alisema Ngerera.
Aliongeza kuwa chama hicho hakimuandai mgombea wa kupambana na Msigwa bali mgombea ambaye atakuwa anaguswa na matatizo ya wananchi na aweza kuyaishi.
Msigwa amewahi kueleza kuwa kutokana na kazi nzuri anayoifanya katika jimbo hilo, haoni mtu anayeweza kumuondoa kupitia sanduku la kura na kwamba wanachopanga hakiwezi kufanikiwa.