Ujumbe kutoka Taasisi ya Uhamasishaji, Uwazi na Uwajibikaji katika Rasilimali Madini na Gesi Asilia nchini Ghana – GHEITI, umefurahishwa na utekelezaji wa mpango wa Uhamasishaji, Uwazi na Uwajibikaji jinsi unavyotekelezwa nchini Tanzania katika mnyororo wa maendeleo ya sekta ya Madini.
Hayo yamesemwa na Mwenyekiti Mwenza wa GHEIT, Dkt. Steve Manteaw mapema baada ya kupokea taarifa kutoka kwa mwenyekiti wa Taasisi ya Uhamasishaji, Uwazi na Uwajibikaji katika Tasnia ya Uziduaji Rasilimali Madini, Gesi Asilia na Mafuta (TEITI) katika mkutano wa kubadilishana uzoefu wa kikazi uliofanyika jijini Dodoma.
Akizungumza katika mkutano huo, Dkt. Manteaw amesema Tanzania kupitia taasisi ya TEITI imekuwa mfano bora kwa kusimamia shughuli za TEITI kwa kutekeleza vigezo vya Kimataifa kama mpango wa Jumuiya ya Kimataifa ya Uwazi, Uwajibikaji na Uhamasishaji (EITI) unavyoelekeza kwa nchi wanachama.
Amesema, jumuiya ya EITI inawachama zaidi ya 57 lakini wamevutiwa na Tanzania ambapo inaonekana kuwa nchi ya mfano mzuri katika uwasilishaji wa ripoti zake ukilinganisha na nchi nyingine ambazo ni wanachama, ambapo ujumbe wa watu 11 kutoka taasisi ya GHEITI upo nchini Tanzania kwa ajili ya kujifunza mambo mbalimbali ndani ya Sekta ya Madini.
Kuhusu mchango wa wachimbaji wa madini nchini , ujumbe huo umevutiwa na mchango wa wachimbaji wadogo kwa kufikia asilimia 40 ya mchango wao ndani ya Sekta hii, huku wakihaidi kuwa wakifika nchini Ghana wataishauri Serikali kuiga mipango shirikishi inayotumika Tanzania ili itekelezwa nchini humo.
Kwa upande wake mwenyekiti wa TEITI, Ludovick Utouh amesisitiza kuwa pamoja mabadiliko ya kupiga hatua katika Uwajibikaji, Uwazi na Uhamasisha katika usimamizi Rasilimali Madini, Mafuta na Gesi Asilia itaendelea kutengeneza mifumo yake ya ripoti ya kimtandao ili wadau wa sekta husika ndani na nje nchi wapate taarifa za malipo ya kampuni pamoja na mapato ya Serikali kutoka katika kampuni husika.
Ameongeza kuwa, kwa kuzingatia kanuni za Kimataifa kupitia EITI kwenye sekta ya Uziduaji itazingatia uwazi katika masuala ya mazingira ili kuongeza usimamizi na uwajibikaji wa kimazingira ndani ya sekta hiyo ambapo katika mkutano huo Tanzania imewakilishwa na wataalam kutoka taasisi zilizo chini ya Wizara ya Madini ikiwemo Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), Tume ya Madini, Ofisi ya Kamishna wa Madini, Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.