Wadau wa Habari Tnchini, wanaendelea kuwasilisha mapendekezo mbalimbali ya mabadiliko ya sheria ya habari kwa Serikali, huku wakishauri baadhi ya vipengele vilivyopo kuondolewa kwa kuwa na tafsiri kandamizi dhidi ya watoa huduma katika sekta ya habari.
Baadhi ya Sheria, zilipitishwa rasmi na Bunge Novemba 5 mwaka 2016 na kutiwa saini na aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania, Hayati John Pombe Magufuli Novemba 16, 2016, ambapo wadau wanasema bado zinaminya uhuru wa vyombo vya habari.
“Hatua hii, inafuatia Serikali kutoa mapendekezo juu ya mabadiliko ya sheria ya Huduma za Habari (Media Services Act), 2016 lakini wadau wanapendekeza mabadiliko zaidi kwenye baadhi ya maeneo,” wamesema wadau hao wakiwemo waandishi wa Habari.
Miongoni mwa vifungu ambavyo vinapendekeza kufutwe ni pamoja na Kifungu cha 5 (1) ambacho kinatoa mamlaka kwa Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo kuratibu matangazo yote yanayotoka Serikalini.
Wadau wanasema “changamoto ya kifungu hicho ni Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo kuwa mshauri mkuu wa Serikali kwenye masuala ya habari, uchapishaji na utendaji wa vyombo vya habari.”
Suala jingine linalotoa ukkasi kwa wadau wa Habari ni kudaiwa kumpa mamlaka ya kuratibu masuala ya matangazo jambo ambalo linaweza kutoa upendeleo kwa kunyima matangazo kwenye magazeti ambayo yataonekana kuchapisha habari zenye mtazamo tofauti na Serikali.
Wanasema, kufutwa kwa kifungu hiki kutatoa nafasi kwa taasisi za Serikali kutoa matangazo yao kwa magazeti wanayoona yanafaa wao na yenye kufika maeneo mengi nchini na kuvifanya vyombo vya habari binafsi kunufaika na matangazo hayo.
Kifungu kingine ambacho kinapendekeza kufutwa ni cha 6 na Kanuni ya 8 (3) na 12 ya Sheria za Huduma za Habari ambacho kinaelekeza magazeti na majarida kufanya uhuishaji wa leseni zao kila mwaka tofauti na utaratibu wa awali wa leseni ya kudumu.
Wanasema, “Changamoto ya kifungu hiki ni Uhuishaji wa leseni za uchapishaji wa magazeti kila mwaka unaweza kutumiwa na Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo kama rungu la kunyima usajili kwa baadhi ya magazeti au majarida ambayo yatakuwa na mtazamo tofauti na Serikali.”
Wametaja utekelezaji wa sheria hiyo kwa kuitolea mfano nchi ya Ghana ambayo haina usajili unaohitajika ili kuendesha biashara ya vyombo vya habari, kama inavyoonyeshwa kwenye Ibara ya 162(3) ya Katiba ya Ghana ya mwaka 1992.
Kifungu kingine cha sheria hii amabcho wadau wananpendekeza kifutwe ni Kifungu cha 7 (2) (b)
(iv) cha Sheria ya Huduma za Habari, ambacho kinatoa maelekezo kwa vyombo vya habari binafsi kuchapisha habari zenye umuhimu kwa Taifa kwa maelekezo ya Serikali.
Wadau wanasema, “Changamoto ya kifungu hiki ni kwamba Kifungu hiki cha Sheria kinaingilia uhuru wa uhariri na hasa kwenye vyombo vya habari vya binafsi, hivyo kikifutwa kitawezesha maamuzi ya kihariri kuzingatia vigezo vya taaluma bila kuathiriwa na maamrisho yasiyo ya kitaaluma.”