Jana, Juni 21, 2023 kwa mara nyingine watu watano walifariki dunia na wengine kadhaa kujeruhiwa baada basi la New Force walilokuwa wakisafiria kupata ajali na kuanguka wakati likijaribu kulipita gari jingine katika kijiji cha Igando kilichopo Kata ya Luduga, Wilayani Wanging’ombe Mkoani wa Njombe.
Taarifa hizi zilishitua Taifa hasa baada ya kumsikia Kamanda wa Polisi Mkoa wa Njombe, John Imori, akisema basi hilo lenye namba za usajili T 173 DZU, baada ya jaribio hilo lilipoteza uelekeo kisha kugonga daraja na kuingia mtaroni.
Kamanda imori alisema, “Basi la New Force lilikuwa linatoka Dar es salaam kwenda Rukwa, lilipofika Igando kuna sehemu ya daraja likawa linataka ‘kuovartake’ likapoteza uelekeo likagonga daraja likaingia mtaroni, tupo eneo la tukio kwa sasa hatujajua majeruhi ni wangapi lakini kuna maiti za Wanaume wanne na Mtoto mmoja.”
Leo Juni 22, 2023 pia tumesikia kwamba idadi ya waliofariki kwenye ajali ya basi ya New Force iliyotokea katika Kijiji cha Igando kilichopo Kata ya Luduga Wilayani Wanging’ombe Mkoani wa Njombe imefikia saba na majeruhi 48 huku wengi wakijiuliza kwanini ajali za barabarani kila mara? na vifo hivi mpaka lini?
Nadhani umefika wakati sasa iwepo haja ya Mamlaka husika za Barabara (TANROADS & TARURA), kuwa na utaratibu wa kutoa elimu ya usalama Barabarani kwa Madereva, ili kufahamu sababu za muundo (Design) ya Barabara husika kuwa hivyo ilivyo.
Ujenzi wa Barabara.
Mara nyingi zinapojengwa barabara mpya au hata kuboreshwa zile zilizopo kuna namna ambavyo barabara hizo hujengwa na hivyo kupelekea mishangao kwa watumiaji wa barabara na watengenezaji wenyewe wa barabara.
Wakati mwingine, wakati watumiaji wa barabara wanaona kama msanifu (designer) wa barabara au mkandarasi (contractor) amekosea katika kuijenga barabara husika, wahandishi wa barabara au wakala wa barabara anaona barabara haina makosa yoyote na inakidhi haja ya kazi au matumizi ya barabara husika huku akimshangaa dereva.
Mifano hai;
(i) namna michoro ya barabara inayokataza au kuruhusu kuovateki ilivyochorwa, (ii) namna au maana ya alama mahususi zilizosimikwa eneo husika, (iii) umbile la barabara la mahali husika, mfano kwa nini wameweka kona badala ya kunyoosha moja kwa moja? Kwa nini wameweka round about kama pale mikumi badala ya kuweka rasta pekee?
(iv) Chaguo la aina ya matuta yanayowekwa barabarani mfano, yale matuta ya ugomvi (kubwaaa limerefuka juu) tofauti na lile lililokaa kama kitanda (flat bed) nk. na elimu hii issishie kubaki kwa wahandisi tu nadhani ishuke hadi kwa madereva na watumiaji wengine wa barabara.
Lakini pia hata wasimamizi wa sheria. Imani yangu inanituma kwamba kupatikana kwa maarifa haya kwa madereva kutawafanya waendeshe pia kwa tahadhari barabarani, akijua kwa nini barabara eneo hili ipo hivi ilivyo huenda ikasaidia. Kinaweza hata kuanzishwa kipindi redioni au kwenye TV cha ‘IJUE BARABARA YAKO’.
Muundo wa kipindi.
Kipindi hiki cha Luninga, kiwe kinazungumziwa barabara tu na taswira zake, kama hivyo michoro, mikunjo, miinuko, alama, nk, na katika vitu hivyo dereva anategemewa afanye nini?
Umuhimu pia unakuja kwa sababu madereva wengi sana hawako vizuri sio tu kwenye kuelewa michoro ya barabarani bali hata kuelewa sababu za kwa nini mfano kipande fulani cha barabara ni kipana wakati sehemu nyingine ni chembamba, au ni kwa nini sehemu fulani kuna alama ya 50 lakini hakuna makazi, nk.
Kwa ufupi inahitajika elimu kuhusu ‘USALAMA WA BARABARA (SAFETY OF THE ROAD)* tofauti na ile ya *USALAMA BARABARANI (ROAD SAFETY)’ au kwa lugha nyingine “kuwa salama barabarani”.
Barabara salama ni ipi na kipi kinafanya barabara kuwa salama, kwamba ukiona hakipo ujue barabara hiyo ni hatari kwa hiyo uongeze tahadhari. Lakini, elimu iende mbali zaidi kueleza ni kwa jinsi gani muundo fulani wa barabara unaathiri spidi au uwiano wa gari barabarani.
Makala hii, imeandaliwa kwa msaada wa vyanzo mbalimbali na ‘CREDIT’ ziende kwa Admin wa RSA.