Kiungo Kutoka nchini Nigeria na Klabu ya Coastal Union Victor Patrick Akpan, amesema kwa sasa hana mpango wa kufikiria usajili wa kuelekea msimu ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara, badala yake amejikita katika mawazo ya kuisaidia klabu yake kumaliza vizuri msimu huu 2021/22.
Akpan ambaye amecheza Coastal Union kwa mafanikio makubwa msimu huu, anatajwa kumalizana na klabu ya Simba SC, ambayo kwa sasa inasaka wachezaji watakaounda kikosi kitakachorejesha heshima ya Ubingwa wa Tanzania Bara na kuvuka hatua ya Robo Fainali kwenye michuano ya Kimataifa msimu ujao.
Kiungo huyo amesesema kwa sasa ni mapema mno kuanza kufikiria usajili ambao anahusishwa nao, kwani bado anajitambua ni mchezaji halali wa Coastal Union, hivyo hana budi kuendelea kupambana kwa maslahi ya klabu hiyo ya jijini Tanga.
“Sina muda wa kuanza kufikiria usajili ambao unahusisha na mimi kwa sasa, jukumu langu ni kushirikina na wenzangu hapa Coastal Union ili tuweze kumaliza msimu huu salama,”
“Tuna michezo miwili imebaki ya Ligi Kuu, pia tuna jukumu zito sana la kucheza Fainali ya Kombe la Shirikisho ‘ASFC’ kule Arusha, litakua jambo la kipuuzi kwangu kuanza kufikiria usajili ambao tayari umeshaanza kwa baadhi ya klabu za Tanzania.” Amesema Akpan
Alipoulizwa kuhusu Simba SC, kiungo huyo amesema anaiheshimu klabu hiyo kwa sababu ni klabu kubwa kwa Tanzania, imejiwekea heshima kubwa Barani Afrika kwa mafanikio iliyoyapata.
“Simba SC ni klabu kubwa kwa hapa Tanzania, imejiwekea heshima kubwa sana Barani Afrika, hivyo ndivyo ninavyoweza kusema kuhusu Simba SC.”
Akpan mwenye umri wa miaka 23 alisajiliwa Coastala Union mwanzoni mwa msimu huu kutoka JKU ya Zanzibar aliyojiunga nayo mwaka 2018, akitokea nchini kwao Nigeria.