Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Sharif Hamad Seif amemlaumu msajili wa vyama vya Siasa nchini Jaji Francis Mutungi kwa kushirikiana na Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) kwa kuunda bodi ya wadhamini feki wa chama hicho.
Ameyasema hayo mapema hii leo Jijini Dar es salaam alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari, amesema kuwa wamefanya hivyo ili kuweza kumsaidia Prof. Lipumba ambaye alijiuzuru kwa matakwa yake mwenyewe.
Amesema kuwa RITA imepata shinikizo kusajili wajumbe feki wa Bodi ya wadhamini wa CUF kwa kutumia majina yaliyowasilishwa na Prof. Ibrahimu Lipumba ili kuhujumu majina halali yaliyopitishwa na Baraza Kuu la Uongozi wa la Taifa kupitia kikao chake kilichofanyika makao makuu ya chama Zanzibar.
“Tarehe 27, Machi 2017 Wakala ulipokea maombi ya Usajili wa Bodi mpya ya Wadhamini ya CUF, kwa mujibu wa usajili maombi hayo hupitiwa kwaajili ya kujiridhisha na sababu ya mabadiliko hayo, ili kuhakikisha kama taratibu zilifuatwa, haya yote hayakufanyika,”amesema Maalim Seif.
Hata hivyo, ameongeza kuwa hujuma iliyofanywa na RITA kwa kushirikiana na Msajili wa vyama vya Siasa nchini na Prof. Lipumba haiwezi kusaidia chochote katika kukiimarisha chama hicho.