Jeshi la Polisi kanda maalum Dar es salaam limetoa siku 3 kwa Sheikh Issa Ponda kujisalimisha na kuhojiwa kuhusu tuhuma zinazomkabili na iwapo hatafanya hivyo watamchukulia sheria stahiki.
Hayo yamesemwa hii leo na Kamishna wa Kanda Maalumu, Kamanda Lazaro Mambosasa alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ambapo ametoa siku tatu kwa sheikh huyo awe amejisalimisha vinginevyo hatua stahiki zitachuliwa dhidi yake.
“Ametenda makosa ya jinai kama uchochezi, lakini pia amekuwa anatoa lugha ambazo ni za kejeli, dhidi ya serikali, anatufutwa na kama unamjua mwambie ajisalimishe ili tuweze kumhoji, kukimbia hakutomsaidia, tukiona kuna kosa la jinai tutampeleka mahakamani kama hana tutamwachia, mimi nampa siku tatu lakini akija leo ni nzuri zaidi, nampa siku 3 ajitokeze mwenyewe aweze kuhojiwa, vinginevyo hatakuwa salama,” amesema Mambosasa
Hata hivyo, Mambosasa ameongeza kuwa hapo jana Jeshi la polisi lilivamia mkutano wa Sheikh Ponda aliokuwa anafanya na waandishi wa habari jijini Dar es salaam, na kufanikiwa kukamata baadhi ya watu wakiwemo waandishi wa habari ambao walikuwepo kwenye mkutano huo.