Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni ameendelea kuwasisitizia watanzania kuacha kurubuniwa kiakili na baadhi ya watu ambao hawaitakii mema Tanzania.
Amesema kuwa wale wote watakao kubali kufanya maandamano kwa madai kuwa wanataka mabadiliko ya uongozi hawatapona hivyo ni bora wakaachana na mpango huo.
Ameyasema hayo jijini Dar es salaam wakati wa uzinduzi wa vituo sita vya polisi vinavyo hamashika katika Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, ambapo amesema wapo watu wachache wanaotaka kuwapotosha vijana kuacha kuchangamkia fursa za maendeleo na kutaka waingie katika maandamano yasioyokuwa na tija ndani yake.
“Katika kipindi hichi wakati nchi yetu inaelekea katika muelekeo mzuri wa kiuchumi na kwamba agenda nyingi zilizokuwa kero wa wananchi zimeweza kutatuliwa chini ya uongozi wa awamu ya tano ila kuna baadhi ya watu waliopo ndani ya nchi na wengine wanaweza kuwepo nje ya Tanzania ambao ni maadui wa mafanikio ambao wanataka sasa kututoa katika mstari uliyonyooka kwa kuibua agenda za kipuuzi, kitoto na zisizokuwa za msingi. Mimi nasema nafasi hiyo hawana,”amesema Masauni