KATIBU wa zamani wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Deus Seif, na Mtunza Hazina Abubakar Allawi, wamehukukiwa kutumikia kifungo cha miezi sita gerezani na kurudisha kiasi cha Shilingi Milioni 13,790,000 baada ya kupatikana na hatia ya makosa mawili ya matumizi mabaya ya madaraka na kujipatia zaidi ya Sh. milioni 13 kinyume cha sheria.
Akisoma hukumu hiyo, Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Richard Kabate amesema ameridhika na ushahidi uliotolewa na mashahidi wa upande wa mashtaka ambao umeweza kuthibitisha kuwa washtakiwa wametenda makosa hayo.
Kabla ya kusoma hukumu ya washtakiwa, Hakimu Kabate aliuliza upande wa mashtaka kama walikuwa na lolote la kusema ambapo Wakili wa Serikali, Imani Mitume akadai kutokuwa na kumbukumbu za makosa ya nyuma za washtakiwa hao.
“Mheshimiwa hatuna kumbukumbu na makosa ya nyuma ya washtakiwa, lakini kulingana na makosa waliyoyatenda na kulingana na nafasi zao kama Viongozi katika Chama cha Walimu kinachopokea michango ya Walimu waliowaamini tunaomba wapewe adhabu kali,” alisema Wakili Mitume.
Akiendelea na hoja zake mbele ya Mahakama, Wakili huyo pia aliomba itoe adhabu kali kwa washtakiwa, ikiwemo kurejesha fedha zote zilizopotea ili iwe fundisho kwa wengine.
Katika utetezi wake, mshtakiwa wa kwanza aliiomba Mahakama impunguzie adhabu kwa kuwa anasumbuliwa na sukari pamoja na shinikizo la damu, na kwamba mke pia anasumbuliwa na maradhi ya aina hiyo.
Aliendelea kudai kuwa, anaishi na mama yake na pia ana watoto wanne ambao wote wanamtegemea na wote wako shule, huku mshtakiwa wa pili kupitia wakili wake Nashon Nkungu akiomba mteja wake apupunguziwe adhabu kwa kuwa wote ni wakosaji wa mara ya kwanza.
“Mheshimiwa mshtakiwa ni mtu mzima anasumbuliwa na maradhi ya sukari na shinikizo la damu hivyo anahitaji kuwa kwenye mazingira mazuri pia anamke na watoto sita ambao wote wanamtegemea yeye na pia washtakiwa wanalitumikia Taifa na walishtakiwa wakiwa wanakitumia Chama cha Walimu walichoakianzisha na kukisimamia kwa nia njema,” alisema Wakili.
Akijibu hoja hizo, Hakimu Kabate amesema “Kwa kuwa imesemwa wazi kuwa hawana makosa mengine, pamoja na makosa haya si kwamba hawana mazuri waliyowahi kufanya makosa yao yanaweza kuwa yalitokana na ukosefu wa umakini hivyo wakateleza kidogo,”
Kabate ameongeza kuwa “Kwa mujibu wa sheria hii mshtakiwa wa kwanza nakuhukumu kifungo cha miezi sita jela kwa makosa yote mawili, ukimaliza utatakiwa kulipa fidia ya Sh 7,590,000 kwa CWT na mshtakiwa wa pili nakuhukumiwa kifungo cha miezi sita jela na ukitoka utalipa fidia ya milioni 6.2 kwa CWT.”
Awali, ilidaiwa mbele ya Mahakama kuwa washtakiwa walitenda makosa hayo kati ya Oktoba 3 hadi Novemba 6, 2018 jijini Dar es Salaam, wakiwa watumishi wa CWT, kwa kutumia madaraka yao vibaya na kujipatia kiasi cha Shilingi Milioni 13,930,963 kwa manufaa binafsi.
Katika shitaka la pili, ilidaiwa kuwa katika tarehe na eneo hilo, washtakiwa walichepusha kiasi hicho cha fedha mali ya CWT kwa kutumia nafasi walizo nazo, huku kesi hiyo upande wa mashtaka ukiongozwa na Wakili Imani Nitume sambamba na mashahidi wanane na vielelezo 12.