Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu, Ummy Nderiananga amewakumbusha vijana kuendelea kuwa mstari wa mbele katika mapambano dhidi ya Maambukizi ya Virusi vya UKIMWI kwa kuzingatia ndilo kundi linaloongoza kwa maambukizi mapya nchini.
Ummy ameyasema hayo wakati akifungua Kongamano la Kitaifa la Kisayansi kuhusu maadhimisho ya Siku ya UKIMWI kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Jenista Mhagama na kusema Kongamano hilo litafanyika kwa siku mbili tarehe 27 hadi 28 Novemba, 2023 Mkoani Morogoro.
Kongamano hilo lilihudhuriwa na wadau mbalimbali ikiwemo Mwakilishi Mkazi wa Umoja wa Mataifa nchini Tanzania, Mwakilishi Mkazi USAID, Wadau wa Maendeleo, Viongozi wa Mkoa wa Morogoro, Wajumbe wa Bodi ya ATF, Baraza la Watu Wanaoishi na VVU Nchini – NACOPHA, Watekelezaji wa Afua za Kudhibiti UKIMWI, Viongozi wa Vyama vya Siasa na Viongozi wa Dini ikiwa ni sehemu ya Maadhimisho ya kuelekea Siku ya UKIMWI Duniani mwaka huu.
Aidha lengo kuu la Kongamano hilo la Kitaifa ni kutathimini mafanikio, changamoto na mweleko wa Taifa katika kutekeleza Lengo la kutokomeza UKIMWI nchini ifikapo mwaka 2030 pamoja na kutoa taarifa za kisayansi zitakazoboresha afua za masuala ya UKIMWI.
“Kauli Mbiu ya mwaka huu ya Siku ya UKIMWI Duniani ambayo pia ni kauli mbiu ya Kongamano letu ni “JAMII IONGOZE KUTOKOMEZA UKIMWI”. Hakika Kauli mbiu hii imekuja wakati sahihi ambapo kama taifa tunahitaji kuihamasisha jamii kuwa mstari wa mbele kuweza kutoa mchango wake katika kufikia azma ya kutokomeza UKIMWI tukianza na kuzuia maambukizi mapya kwa vijana wetu hasa Wasichana.