Mkutano unaohusu masuala ya Ulinzi na Usalama wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) umefanyika Maputo, Msumbiji chini ya Mwenyekiti wake ambaye pia ni Rais wa Msumbiji, Fellipe Nyusi.
Viongozi wa mataifa ya SADC wametoa taarifa ya pamoja inayoelezea wasiwasi wao kuhusiana na machafuko yanayofanywa na makundi ya itikadi kali yanayoendelea kujitokeza kaskazini mwa Msumbiji na kusababisha maelfu ya watu kufa na wengine wengi kuyakimbia makazi yao.
Wakuu hao wamelaani mashambulizi hayo ya kigaidi na kwa pamoja wametoa msimamo mkali wakisema mashambulizi kama hayo hayakubaliki na hayatakiwi kuendelea.
Marais kutoka nchi tano ikiwemo Afrika Kusini, Botswana, Malawi na Mwenyeji Msumbiji wamehudhuria ambapo kwa upande wa Tanzania Rais wa Zanzibar Dkt. Hussein Mwinyi amemuwakilisha Rais Samia Suluhu katika Mkutano huo.
Rais Nyusi amezishukuru nchi Wanachama na kuwaomba kuendelea kuzidisha ushirikiano katika kuhakikisha hali ya usalama inaimarishwa zaidi sio tu katika eneo la Cabo Delgado lililokumbwa na tishio la ugaidi, bali kwenye Jumuiya yote.
Wakuu hao wanatarajiwa kukutana tena Aprili 29 kwenye Mkutano mwingine wa kilele wa kuujadili mzozo huo.