Marekani imezifunga tovuti za habari zenye mafungamano na Iran
Mamlaka nchini Marekani imezifungia tovuti za habari zenye mafungamano na serikali ya Iran kwa tuhuma za kueneza habari za upotoshaji.
Idara ya sheria nchini humo imesema tovuti 33 zilizofungiwa zilitumiwa na vituo vya redio na televisheni ya serikali ya Iran, ambavyo serikali ya Marekani inavituhumu kwa kueneza habari za uwongo.
Marekani imesema tovuti tatu kati ya hizo zilikuwa zinaendeshwa na kundi la Kata’ib Hizballah, ambalo zaidi ya muongo mmoja uliopita lilitajwa kuwa kundi la kigaidi.
Kundi hilo ni tofauti na lile la wanamgambo wa Hezbollah ambalo tovuti zake za habari zinaendelea kufanya kazi.
Aidha, imevituhumu vyombo hivyo kuwa vilisambaza habari zilizokuwa na nia ya kuwapotosha wapiga kura wa Marekani kabla ya uchaguzi wa Rais wa Marekani mwaka 2020.
Tovuti hizo 33 zilikuwa zinamilikiwa na muungano wa redio na televisheni za kiislamu nchini Iran IRTVU unaodhibitiwa na kitengo cha jeshi la mapinduzi la iran kinachosimamia mapambano dhidi ya wapiganaji wa kikurdi IRGC.