Wizara ya Viwanda na Biashara imekutana na wadau wa sekta binafsi jijini Dar es Salaam kujadili mapitio ya Sera ya Maendeleo ya Viwanda Vidogo na Biashara Ndogo huku ikiwa ni mchakato wa maboresho wa sera hiyo muhimu nchini.
Akizungumza na wadau hao wakati akizindua mkutano huo, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Dkt. Hashir Abadallah amewataka washiriki hao kupitia kwa makini rasimu hiyo na kutoa mapendekezo yatakayoiboresha zaidi ili kupata sera inayoendana na mabadiliko ya sayansi na teknolojia.
Aidha amewataka wadau hao kutambua kuwa Sera ya Maendeleo ya Viwanda Vidogo na Biashara Ndogo’ nchini inayoandaliwa inabeba wajasiriamali zaidi ya milioni 4.5 hivyo inaitaji umakini katika maandalizi yake ili kuja na suluhisho ya changamoto nyingi kwa wajasiliamali.
“Kwa bahati nzuri zaidi, sekta hii ndio inayobeba takribani asilimia 98 ya viwanda vyote nchini. Hii ni faraja kwa kuwa malighafi za nchi yetu hasa za wakulima zinapata masoko katika viwanda hivyo hasa ikizingatiwa viwanda vya sekta hii vimesambaa nchini kote na vingi vikijihusisha katika uongezaji thamani hasa wa mazao ya kilimo,” Amesema naibu katibu Abdallah.
Halikadhaalika Naibu Katibu Mkuu amesema kuwa Serikali inatambua na kuthamini umuhimu wa sekta binafsi nchini hususan thamani ya uendelezaji wajasiriamali katika kuendeleza shughuli za uchumi wa nchi.