Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa imesema vyama vya TLP na UDP vilishasitisha mpango wa kumuunga mkono mgombea urais wa Tanzania kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Dkt. John Magufuli kwa sababu havikufuata kanuni na sheria za uchaguzi.
Naibu msajili wa vyama vya siasa, Sisty Nyahoza amesema, waliwaambia TLP na UDP suala hilo lina utaratibu ambao walitakiwa kuufuata, na walipoona hawajafuata vyama hivyo vimekaa kimya na havisikiki tena.
Ameongeza kuwa UDP wameendelea na kazi zao za kampeni, wakiwa na mgombea wao na wanatangaza sera za chama chao huku TLP ambao waliweka mabango wameyatoa na wanaendelea na kampeni zao.
Nyahoza amesisitiza suala la vyama kuwa n usikivu kufuata maelekezo wanayopewa na kuzingatia sheria na kanuni.
“Kwa hiyo Vyama ni sikivu, vile ambavyo sio sikivu wawe wasikivu na kuzingatia Sheria na Kanuni maana kama Mgombea wa Chama chako asipokuwa msikivu, akishinda kwenye uchaguzi itakuwaje?” amesema Nyahoza.