Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mwanaidi Ali Khamis amevishauri vyuo vya elimu ya juu nchini kuhakikisha vinasimamia malezi na maadili ya wanafunzi wao kutokana na wengi wao kujiunga na masomo wakiwa na umri mdogo.
Ameyasema hayo wakati wa hafla ya kuweka jiwe la msingi la miundombinu ya Chuo Cha Mipango ya Maendeleo Vijijini Kituo cha Mafunzo Kanda ya Ziwa – Mwanza kinachojengwa katika kijiji cha Kitumba, wilayani Magu mkoani Mwanza kwa gharama ya zaidi ya shilingi Bilioni 2.
Aidha amekishauri Chuo kuboresha mitaala itakayovutia wanafunzi wengi zaidi wakiwemo wanaotoka nje ya nchi zikiwemo nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki na Nchi za maendeleo Kusini mwa Jangwa la Sahara (SADC) pamoja na kuanzisha vituo vya umahiri ili kuwapa vijana ujuzi utakaosaidia wajiajiri na kujipatia kipato.
Mwanaidi amekiasa Chuo hicho kuhakikisha kuwa kinafanya tafiti mbalimbali zitakazoibua suluhu za changamoto zinazokwaza maendeleo ya wananchi hususani wa vijijini na kuziandika tafiti hizo kwa lugha rahisi ya Kiswahili ili tafiti hizo ziweze kuwanufaisha wananchi na kuchangia kujikwamua kiuchumi.