Waziri wa Viwanda na Biashara, Dkt. Ashatu Kijaji ameonesha kukerwa na uendeleaji wa kufungwa kwa Biashara na Viwanda kupitia Taasisi za Serikali zenye mamlaka ya udhibiti Viwanda na Biashara, kutokana na changamoto mbalimbali za Wafanyabiashara.

Dkt. Kijaji ameyasema hayo wakati akifungua mkutano ulioambatana na Maonyesho ya biashara ya Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni BRELA na Wadau wake uliofanyika jijini Dar es Salaam na kudai kuwa shughuli za Biashara na Viwanda zinaendelea kuchangia ukuaji wa uchumi wa Taifa na sheria ilizuia hatua hiyo.

Waziri wa Viwanda na Biashara, Dkt. Ashatu Kijaji.

Amesema, katika mwaka wa fedha wa 2023/2024 kupitia sheria ya fedha ya 2023, jumla ya sheria na kanuni 17 zimefanyiwa marekebisho, ikiweza kupunguza na kufuta jumla ya tozo, ada na faini 97 kwa lengo la kuhakikisha mazingira ya ufanyaji Biashara yanakuwa bora kabisa.

“Hapa naomba ni sisitize na kutoa rai kwa mamlaka zote za serikali za udhibiti ziendelee kuruhusu biashara zifanye kazi hata kama kuna jambo hatukubaliani kati yetu lakini wakati tunashughulikia jambo lile hakuna sababu ya kusitisha shughuli za biashara kwani kusitisha biashara ni kusimamisha uchumi wa nchi,” amesema Dkt. Kijaji.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya ya ushauri ya BRELA Prof. Neema Mori amesema Lengo kuu la Mkutano wa BRELA na wadau wake ni Kuimarisha mawasiliano baina ya BRELA na Wadau wake ili kujenga uelewa wa huduma zinazotolewa na BRELA pamoja na kupata mrejesho wa ubora wa huduma hizo.

Naye Afisa Mtendaji Mkuu wa BRELA, Godfrey Nyaisa amesema mkutano huo utakuwa ukifanyika kila mwaka na ushirikishwaji utazidi kuwa mpana zaidi ukiambatana na mijadala itakayohusisha shughuli za BRELA ikiwemo Usajili wa Makampuni, Majina ya Biashara, Miliki Ubunifu na Utoaji Leseni.

Iran kuwekeza sekta ya Mafuta na Gesi nchini
Wakutana kujadili uondoaji vikwazo sekta ya Madini