Waasi wa M23 ambao wanadhibiti maeneo mengi ya mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo DRC, wameahidi kuondoka kwenye eneo la kimkakati la mapambano karibu na mji wa Goma.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa Desemba 23, 2022 , M23 imetangaza kwamba itaondoka kwenye mji wa Kibumba, ulioko umbali wa kilomita 20 kutoka Goma.
Mji wa Kibumba kwa sasa ni eneo la mapambano kati ya M23 na majeshi ya serikali ya DRC huku M23 ikisema kuwa itaukabidhi mji wa Kibumba kwa kikosi cha jeshi cha Jumuia ya Afrika Mashariki kama ishara ya nia njema.
Hatua hiyo, inajiri baada ya mazungumzo ya amani ya hivi karibuni yaliyofanyika kwenye mji mkuu wa Angola, Luanda ambapo pia kundi hilo limeitaka serikali ya Kongo kuitumia fursa hii kwa mikono miwili.